Yale yale! Simba kama Yanga


Kiungo wa timu ya Simba,Kanu Mbiyavanga(kushoto) akiwatoka wachezaji wa URA ya Uganda Agaba Oscar(katikati) na Feni Ali,katika mechi ya kuwania kombe la Kagame,kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana,Simba ilifungwa 2-0

JINAMIZI la kufanya vibaya kwenye michuano ya Kagame limeendelea kuzikumba timu za Tanzania, baada ya Simba kuchapwa mabao 2-0 na URA huku Azam wakilazimisha sare ya 1-1 na Mafunzo ya Zanzibar. Kipigo hicho cha Simba kimekuja siku moja baada ya watani zao Yanga kuchapwa 2-0 na Atletico ya Burundi kwenye mchezo wa ufunguzi.

Wakati wawakilishi hao wa Tanzania wakisuasua jana timu ya Vita Club ya DR Congo iliichakaza Ports ya Djibouti mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Azam Chamazi. Mabingwa wa Uganda, URA katika mechi dhidi ya Simba walipata ushindi huo kwa kufunga bao kila kipindi kupitia kwa mshambuliaji wake Feni Ally ambaye alifunga mabao yote kwa kichwa huku bao la kwanza akifunga dakika ya 11.

Ushindi huo umeifanya URA kukamata nafasi ya pili nyuma ya Vita Club kwa tofauti ya mabao baada ya Wakongo hao kuisambaratisha Ports kwa mabao 7-0. Katika mechi kati ya Vita Club na Ports, mshambuliaji Etekiama Taddy alifunga mabao manne peke yake huku Ngudikama Emmanuel akifunga mawili na Basilisa Makola akifunga bao moja.

Katika Uwanja wa Taifa, Simba walianza mchezo kwa kasi na dakika ya 5 shuti la Felix Sunzu lilipanguliwa kwa ustadi mkubwa na kipa wa URA, Mugabi Yasin. Mabingwa wa Uganda waliamka na kuanza kulishambulia lango la Simba, ambapo dakika ya 6, kipa Juma Kaseja alitumia uzoefu wake kudaka shuti la Yutimba Yayo wa URA.

Simba walijaribu kujibu mapigo dakika ya19 baada ya Danny Mrwanda kuwatoka mabeki wa URA, lakini shuti lake lilikwenda nje, pia katika dakika ya 38 alipiga shuti kali ambalo lilipanguliwa vizuri na kipa Mugabi. Katika mechi hiyo beki aliyetemwa na Simba, Derrick Walyula aliyejiunga na URA hivi karibuni alicheza kwa kiwango cha juu na kumdhibiti vizuri mshambuliaji Sunzu.

URA walitawala vizuri sehemu ya kiungo wakiongozwa na Kyeyuni na Owen Kasule, ambapo walifanikiwa kuwadhibiti Nkanu Mbiyavanga na Amri Kiemba. Dakika ya 47, Kaseja alifanya kosa baada ya kutoka na kuucheza mpira kwa kichwa uliotua mguuni kwa Kyeyuni, lakini shuti la kiungo huyo lilipaa juu.

Pia katika dakika ya 72 mshambuliaji Robert Ssentongo alimzidi ujanja beki Obadia Mungusa na kupiga shuti, lakini kipa Kaseja alikuwa makini na kulipangua kuwa kona. Wakati Simba wakisaka bao la kusawazisha URA walifanya shambulizi la kustukiza kupitia winga ya kulia aliyepiga krosi nzuri iliyotua kichwani kwa mkongwe Simeon Masaba aliyedundisha mpira chini na kujaa wavuni dakika 90 na kufanya mchezo kumalizika 2-0.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic aliwapumzisha Danny Mrwanda, Nkanu Mbiyavanga, Kiemba na kuwaingiza Abdallah Juma, Haruna Moshi na Uhuru Selemani. Wakati kocha wa URA, Isabirye Alex alimtoa Kyeyune, Lutimba Yayo, Kasule na kumwingiza Bagala Sula, Wejuli Osman na Mubiru Samwel.

Chamazi; Azam wakicheza kwenye Uwanja wake waliduwazwa na Mafunzo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1. Mshambuliaji John Boko aliendelea kuwa na makali yake ya kuzifumania nyavu baada ya kuipatia bao timu yake ya Azam katika dakika ya 27, ambapo alitoka mabeki wa Mafunzo, Yusufu Juma na Said Mussa na kufunga bao hilo.

Katika mechi hiyo kiungo Seleman Kassim wa Mafunzo alikosa bao akiwa yeye na kipa wa Azam, Deogratus Munishi, ambapo shuti lake lilitoka nje. Mafunzo walisawazisha bao dakika ya 47 mfungaji akiwa Ally Juma na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 1-1. Kwa matokeo hayo Azam sasa watalazimika kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Tusker ya Kenya ili iweze kukata tiketi ya kucheza hatua ya pili.

Chanzo:Mwananchi

Advertisements

Posted on July 16, 2012, in Bongo, Mpira, Mpira kwa Dakika and tagged , , . Bookmark the permalink. Leave a comment.

Comment

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: