Stars yaumia kiume Msumbiji


POULSEN

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imetolewa katika mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2013 baada ya kuchapwa na Msumbiji kwa mikwaju ya penati 7-6 katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto mjini Maputo, Msumbiji.

Kabla ya kupigwa penati hizo mechi hiyo ilimaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1, huku bao la Taifa Stars likifungwa na Aggrey kwa kichwa dakika ya 90 akiunganisha kona ya Amir Maftah.

Katika mchezo wa kwanza Februari  29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya ya 1-1, na sare kama hiyo Msumbiji ilipelekea kupigwa penalti.

Wachezaji wa Stars waliofunga penalti ni Amir Maftah, Shaaban Nditi, Shomary Kapombe, John Boko, Frank Domayo na Mrisho Ngasa, huku Aggrey Morris, Kelvin Yondani na Mbwana Samata wakikosa penalti na kipa Juma Kaseja akipangua penati mbili.

Kwa upande wa Msumbiji penalti zao zilifungwa na Almiro Lobo, Massinga, Martinho, Clesio, Edson, Stelio na Dominguez wakati waliokosa ni Chimomole na Chavango.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi saa 10 za jioni, huku Msumbiji wakishambulia kwa nguvu kupitia upande wa kushoto kwa Taifa Stars.

Kasi hiyo ya Msumbiji ilisababisha Elias Gaspar “Domingues” Pelembe kumpa taabu Erasto Nyoni katika upande wa kushoto.

Msumbiji ‘Mambaz’ walipata bao katika dakika ya 9 mfungaji akiwa Jeremias Sitoe aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Domingues anayechezea klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kabla ya kufungwa bao hilo wachezaji wa Taifa Stars walionekana kupoteana uwanjani, lakini baada ya kufungwa walirudi mchezoni na kutawala sehemu ya kiungo hasa baada ya Shaaban Nditi kurudi nyuma na Frank Domayo kusogea mbele.

Stars walijitahidi kupeleka mashambulizi langoni mwa Msumbiji na dakika ya 24, Samata alipiga shuti dhaifu ambalo lilidakwa na kipa wa Msumbiji Joao Rafael.

Hali iliendelea kuwa ngumu kwa Stars katika kipindi cha kwanza huku wachezaji wake wakipoteza umakini katika ushambuliaji na kushindwa kupeana pasi nzuri.

Katika dakika ya 45 Msumbiji walienda tena katika lango la Stars na kufanya shambulio la kushtukiza, ambapo shuti la Sitoe liligonga mwamba na kurudi uwanjani.

Pia katika dakika ya 46, Msumbiji walifanya shambulizi lingine wakitaka bao la pili, lakini umakini wa Aggrey Morris ulisaidia kwa sababu alilala chini na mpira ukamgonga na kipa Juma Kaseja akawahi kuudaka.

Mpaka mapumziko Msumbiji ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0. Wachezaji Shaaban Nditi, Mwinyi Kazimoto walionekana kutokuwa kwenye kiwango tofauti na Domayo na Ngasa waliocheza vizuri.

Katika kipindi cha kwanza pia tatizo lililokuwa likiwasumbua wachezaji wa Stars ni kushindwa kurudi kwa haraka kuzuia na Msumbiji.

Baada ya kipindi cha pili kuanza Stars walifanya mabadiliko, ambapo alitoka Thomas Ulimwengu na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Moshi ‘Boban’.

Katika kipindi cha pili Msumbiji walianza kwa kutawala sehemu ya kiungo na kuendelea kutafuta njia upande wa kushoto alipokuwa akicheza Nyoni kwa sababu Kazimoto alikuwa hashuki nyuma kumsaidia Nyoni.

Hali hiyo ilisababisha Msumbiji kukosa mabao katika dakika ya 57 na 60.
Kocha Kim Poulsen aliamua kumtoa Kazimoto dakika ya 61 na nafasi yake kuchukuliwa na Amir Maftah ili akamsaidie Nyoni aliyekuwa akisumbuliwa na nyota wa Msumbiji, Dominguez.

Kwa muda mwingi wa kipindi cha pili Stars ilipotea na kushindwa hata kupiga pasi tano sahihi.
Katika dakika ya 69 Stars walifanya shambulio katika lango la Msumbiji, lakini shuti la Ngasa lilidakwa na kipa Joao Rafael, pia baada ya muda mfupi Ngasa alijitahidi kupiga tena shuti kutafuta bao ila lilitoka nje.

Ngasa na Samata katika mechi walishindwa kuchezeshana, ambapo kila mmoja alikuwa akicheza kivyake badala ya kupasiana kurahisisha mashambulizi yao.

Mwishoni mwa kipindi cha pili Stars walifanya tena mabadiliko alitoka Nyoni na nafasi yake ilichukuliwa na John Boko, huku Msumbiji wakimtoa Sitoe na nafasi yake kuchukuliwa na Clesio Bauque.

Dakika ya 80 Samata alichezewa faulo nje ya 18 na Stars kupata faulo, lakini shuti lililopigwa na Aggrey lilidakwa na kipa wa Msumbiji.

Ikiwa mechi inaonekana kumalizika kwa wenyeji kutoka na ushindi, Aggrey Morris aliisawazishia Stars bao kwa kichwa akiunganisha kona ya Amir Maftah na kuwanyamazisha mashabiki wa Msumbiji.

Kwa ushindi iliopata Msumbiji imefanikiwa kuingia raundi ya pili ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini 2013.

Kikosi cha Stars kilikuwa hivi:  Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Kevin Yondani,  Shaabani Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Thomas Ulimwengu/ Haruna Moshi, Mbwana Samata na 15. Mwinyi Kazimoto/Amir Maftah.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Posted on June 18, 2012, in Bongo, Mpira, Mpira kwa Dakika and tagged , . Bookmark the permalink. Leave a comment.

Comment

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: