Yanga, Simba zageuzwa ‘Shamba la Bibi’


Moto magoma

KLABU kongwe za Simba na Yanga za jijini Dar es Salaam, zinaingiza mamilioni ya pesa kila mwaka kupitia viingilio vya uwanjani, lakini kutokana na mlolongo wa makato toka taasisi mbalimbali, zimejikuta zikiambulia kiasi kidogo kulinganisha na kilichovunwa.

Mbali na makato toka taasisi hizo, likiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo huzoa mgao mkubwa, jambo lingine linaloziponza klabu hizo ni kutokuwa na viwanja vyao binafsi ambavyo wangeweza kuvitumia kwa ajili ya mechi zao mbalimbali na hivyo kupunguza makato.

Baadhi ya makato ‘yanayonyonya’ klabu hizo ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF), Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam (DRFA), gharama za uwanja kama ulinzi, usafi, umeme, tiketi nauli za ndani kwa waamuzi na kamishna, posho za kujikimu kamishna na gharama za kuwalipwa wajenzi wa uwanja, kampuni ya China (Beijing Construction).

Yanga pamoja na kumiliki Uwanja wa Kaunda, lakini haufai na hauna kiwango cha kuchezwa mechi za Ligi Kuu, na Simba haina kabisa uwanja wake binafsi zaidi ya kumiliki eneo wanalotarajia kujenga uwanja.
Klabu ya Azam FC iliyoanzishwa miaka ya karibuni ndiyo pekee nchini yenye uwanja wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mechi za Ligi Kuu, hali ambayo imefanya kukwepa baadhi ya makato.

Kwa mfano, msimu wa 20l0/2011 na 2011/2012, mechi nne za Ligi Kuu zilizozikutanisha timu hizo, zilipatikana kiasi cha Sh979.5 milioni lakini baada ya makato kila mmoja akaambulia Sh227.7 milioni tu.
Kiasi hiki walichopata ni kidogo kulinganisha na pesa zilizoingizwa na klabu hizo katika mechi hizo nne baina yao, achilia mbali mechi nyingine za ligi hiyo na michuano mingine ya kimataifa.

Hii ina maana kwamba, klabu hizo zimekuwa ziingiza kiasi kikubwa cha pesa, lakini zimejikutaka zikiambulia kiasi kidogo kutokana na orodha ndefu ya makato.

Katika misimu miwili, Simba na Yanga zilikutana mara nne, mara tatu kwenye Taifa, Dar es Salaam na mara moja Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambapo Yanga ilishinda michezo miwili, sare moja na Simba kushinda mmoja.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mwananchi, mchezo wa kwanza wa timu hizo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Oktoba 18, 2010, ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, zilipatikana Sh138 milioni.

Mapato hayo yalivunja rekodi ya yale ya awali yaliyosomeka Sh105 milioni katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Taifa Stars na Senegal mwaka juzi.

Jumla ya watazamaji 25,000 waliingia uwanjani kwenye mchezo huo kwa kiingilio cha juu Sh30,000 na cha chini 5,000, ambapo kila timu uliambulia Sh33.4 milioni.

Machi 5, 2011 katika mzunguko wa pili, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, ziliingiza Sh243 milioni baada ya kuingia watazamaji 46,539, ambapo kiingilio cha juu kilikuwa Sh30,000 na cha chini Sh3,000. Katika mgao huo kila timu iliambulia Sh51.1 milioni.

Aidha, katika mchezo namba 78 uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Oktoba 29 mwaka jana, timu hizo zilivuna kiasi cha Sh337.5 milioni.

Pesa hizo zilipatikana baada ya kuingia uwanjani watazamaji 53,366 kwa kiingilio cha chini Sh5,000 na kila cha juu zaidi Sh20,000 kwa siti za VIP A. Yanga ilishinda bao 1-0.

Baada ya makato, kila timu iliweka mfukoni kiasi cha Sh77milioni, na mchezo wa mwisho ya Ligi Kuu msimu huu ulikuwa Mei 6, ambapo watazamaji 41,733 waliingia uwanjani.

Kiasi cha Sh260.9 zilipatikana na kila timu ikaweka mfukoni kiasi cha Sh62.6milioni, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga.

Katika misimu hiyo miwili, msimu wa mwaka 2011/2012 ndiyo uliokuwa na mavuno mengi kwa timu hizo kulinganisha na msimu uliotangulia kwa tofauti ya Sh61 milioni.

Akiongelea hali hiyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwasigwa alisema mfumo wa makato wa unaziumiza kwa kiasi kikubwa klabu ambazo msingi mkubwa wa kuziendesha utegemea mapato ya milangoni.

“Kweli makato ni makubwa sana, kuna mlolongo mrefu wa gharama ambazo zinalipwa toka kwenye viingilio. Kwa hali hii, klabu zetu haziwezi kusonga mbele,” alisema Mwasigwa.

Mwasigwa alisema wamezungumza mara kwa mara na TFF kuhusu makato hayo, lakini hakuna ambalo limeweza kufikiwa mpaka sasa. “Tunahitaji mabadiliko yenye kuzinufaisha klabu na siyo kuzinyonya.”

Advertisements

Posted on May 29, 2012, in Mpira and tagged , , . Bookmark the permalink. 2 Comments.

  1. imekaa vibaya sana walaji ni wengi sana katika nchi hii

Comment

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: