Nchunga abwaga manyanga Yanga


nchunga

SIKU moja baada ya kuvamiwa nyumbani kwake usiku wa manane na kundi la watu wasiojulikana Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga amejiuzulu kuiongoza klabu hiyo.

Nchunga alitangaza uamuzi huo wa kujiuzulu jana jijini Dar es Salaam kwenye ofisi yake iliyopo jengo la NSSF Akiba mbele ya waandishi wa habari wachache.

Alisema,”sipo tayari kuona klabu Yanga inahujumiwa kwa vile tu mimi ni kiongozi, Kamati ya Utendaji na wale walioteuliwa chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafaniko zaidi.”

“Kwa hekima nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klabu ninayoipenda hata kama mimi sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu,”alisema Nchunga.

Katika siku za hivi karibuni Nchunga amejikuta kwenye mgogoro mkubwa na Baraza la Wazee la klabu hiyo ambao walikuwa wakimshinikiza ajiuzulu kwa madai kuwa ameisababisha madeni makubwa klabu hiyo ikiwa ni pamoja na mwenendo mbovu wa timu yao huku wakidai wachezaji wamekosa nidhamu.

Pia wazee hao walikuwa wakimlaumu Nchunga kwa kusababisha Yanga kupata matokeo mabovu katika  mchezo dhidi ya watani zao wa jadi Simba walipofungwa mabao 5-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Tanzania bara.

Nchunga akizungumza jana na waandishi wa habari alisema kitendo kinachofanywa na Baraza hilo la Wazee wakiongozwa na Ibrahimu Akilimali ni usaliti mkubwa ulioambatana na matukio mbalimbali yanayoendelea ndani ya klabu hiyo hadi kuupindua uongozi wake.

“Siwatuhumu wachezaji moja kwa moja, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo na Simba inaonyesha kulikuwa na usaliti mkubwa ambao hatukuweza kuubaini mapema,”alisema Nchunga.

“Sioni mantiki kwa hoja kuwa tulifungwa kwa vile wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho, au eti mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao tano,”alisema Nchunga.

Alisema,”kwa wanaoijua Yanga wanafahamu Yanga  imewahi kuwa na madeni makubwa katika hoteli mbalimbali, mawakala wa ndege na baadhi tumeyakuta sisi na kuyalipa, hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwapo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki na bado wachezaji walicheza kwa morali?.”

“Uongozi wangu ndani ya mwaka mmoja tumechukua mataji matatu, ubingwa wa Ligi Kuu, 2011/2012, Kombe la Kagame na Ngao ya Hisani ukiachia mechi ya Mei 6 ambayo tulifungwa magoli matano,”alisema Nchunga.

Alisema,”tumefanikiwa kuboresha mkataba wetu na TBL, tumeingia mkataba na Nexus Ltd ambao inatutafutia wadhamini wa ndani na nje, tumefanya kampeni kupitia mitandao na kukusanya data za wanachama na kusajili wapya lengo likiwa ni kukusanya Sh3,000,000 hadi 8,000,000 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu.”

Nchunga alisema,”hayo yote tulifanya ili kuondokana na utegemezi wa ufadhili wa mtu mmoja na tayari tulishatuma maombi kwa msajili Manispaa ya Ilala ya kuanzisha Saccoss ya Yanga.”

“Utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatutafuna kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuondoa uongozi wa kidemokrasia,”alisema Nchunga akiwa na sura ya huzuni.

Alisema,”baada ya Mapinduzi kushindikana na TFF kuonya, wazee wakiongozwa na Akilimali wamesikika katika kipindi cha michezo cha radio moja wakidai ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza.

Katika hatua nyingine Nchunga pia, alisema jana majira ya saa nane usiku alisikia mbwa wakibweka kwa nguvu huku taa za alamu zikipiga kelele mfululizo kitendo ambacho kilimstua na alipochungulia dirishani aliona kundi la watu wanaokadiriwa kufikia 15 wakiwa kwenye harakati za kutaka kuingia ndani kwake.

“Baada ya kusikia kelele zile za alamu na mbwa tuliwapigia simu walinzi wetu wawili kumbe na wenyewe walikuwa wameshafanya jitihada za kutafuta nguvu kwa walinzi wengine kitendo kile kililiogopesha kundi lile na kukimbilia bondeni, hata hivyo tulipiga simu polisi ambao walifika na kukuta kundi hilo limeshatoweka,”alisema Nchunga.

Alisema,”suala hilo hivi sasa lipo Polisi na upelelezi unaendelea ili kubaini waliohusika katika kitendo kile.”

Chanzo: mwananchi

Advertisements

Posted on May 25, 2012, in Bongo, Mpira and tagged , . Bookmark the permalink. Leave a comment.

Comment

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: